Zitto: Niko tayari

LICHA ya uongozi wa Chadema kutaka wanachama wa chama hicho kuacha kumpa ushirikiano Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, yeye amesema yuko tayari kufanya kazi na kiongozi yeyote wa chama hicho aliye tayari.



Ziito Kabwe
“Mimi niko tayari kufanya kazi na kiongozi yeyote wa Chadema ambaye atakuwa tayari kufanya kazi nami, kwa sababu naamini suala hapa ni ujenzi wa nchi yetu, ni ujenzi wa Taifa letu na naamini hata kama nina mawazo kidogo, lakini ni kwa ajili ya kuiendeleza nchi yetu,” amesema Zitto.


Akihojiwa jana na mtandao wa kijamii wa millardayo.com, Zitto alisema sasa hivi kuna masuala makubwa kuhusu Katiba ya nchi na angependa wananchi wajielekeze huko.


“Sijafurahishwa sana na kinachoendelea hivi sasa, maana yake wananchi wameacha kujadili masuala ya msingi yanayowahusu, nasikitika kuona vyombo vya habari ni habari za Zitto na Chadema, nashukuru jambo hili limekwisha sasa kwa muda huu,” alisema akimaanisha mgogoro na chama chake.


Alisisitiza kuwa bado ni mwanachama wa Chadema, licha ya Katibu Mkuu wa Chama hicho, Dk Wilbrod Slaa, kutoa amri ya watu kumnyima ushirikiano “lakini pale nitakapohitajika nitafanya shughuli za Chadema, nitafanya shughuli za nchi yangu.”




Kuhusu ushindi wake wa juzi mahakamani, alisema si ushindi dhidi ya chama, kwa sababu hawezi kushindana na chama chake, kwa kuwa kimemlea na amekitumikia kwa muda wote, zaidi ya nusu ya umri wake.


“Kwa hiyo salamu ambazo napenda wananchi wazifahamu ni kwamba tunahitaji kuheshimu sana demokrasia na misingi ya haki za binadamu,” alisema.


Akizungumzia uamuzi wa Mahakama, uliotolewa na Jaji John Utamwa, alisema utaweka utaratibu kwamba watu ambao ni wanachama wa vyama hawataonewa, hawatadhulumiwa wala kukandamizwa na watakuwa huru kutoa maoni yao wanapohitaji kufanya hivyo.


“Nataka niseme wazi kabisa kwa Watanzania ambao ni wanachama wa vyama vingine, wasio na vyama na kwa wana Chadema, ushindi huu si dhidi ya Chadema, ni wa Watanzania wote wanaopenda siasa safi na taratibu za utawala bora zifuatwe kwenye taasisi zetu.


“Ni ushindi dhidi ya wanaotaka kukandamiza demokrasia ndani ya vyama, ni ushindi dhidi ya wahafidhina wasiotaka mabadiliko katika vyama,” alisema.